Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina. Kesho, Julai 9, ni miaka 15 tangu Sudan Kusini ipate uhuru wake kutoka Sudan. Hata hivyo, matumaini ya amani yalitikiswa miaka miwili baadaye, mwezi Desemba 2013, baada ya kuzuka kwa mapigano kati ya serikali na makundi pinzani, hali iliyoendelea kuwaathiri mamilioni ya wananchi hadi leo. Katika juhudi za kurejesha amani, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNMISS, kwa ushirikiano na serikali ya jimbo la Equatoria Magharibi, umezindua kampeni mpya iitwayo "Tusikilizeni, Chukueni Hatua Sasa" (Hear Us, Act Now), inayolenga kuimarisha maridhiano, mshikamano wa kijamii na kuwahamasisha vijana kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa amani. Feissal Kirwa, kupitia video ya UNMISS, amefuatilia uzinduzi wa kampeni hiyo na sasa anatuletea mada hii kwa kina.Pia tunakuletea muhtasari wa habari na jifunze Kiswahili..Ripoti mpya ya hali ya saratani duniani kwa mwaka huu wa 2026 iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani (WHO) na shirika lake tanzu la utafiti wa saratani, IARC ikionya kuwa unyanyapaa ni moja ya vikwazo vya kutokomeza saratani wakati huu idadi ya wagonjwa ikikadiriwa kuongezeka maradufu ifikapo 2050, manusura wa saratani ya titi Abigael Hartz mkazi wa Ireland lakini anatokea Nigeria anasimulia alichoshuhudia alipotembelea hospitali moja ya kupima saratani Nigeria.Wiki mbili tangu matetemeko makubwa ya ardhi yapige mji mkuu wa Venezuela, Caracas na viunga vyake, idadi ya waliokufa imeripotiwa kufikia 3,685, majeruhi 16,740 na waliookolewa 6,462, Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Msaada wa Dharura, OCHA, Tom Fletcher yuko nchini humo na anasema.. “Hapa ni La Guaira, ambalo kwa hakika ndilo eneo lililokumbwa zaidi na janga hili. Nimekutana na mama mmoja aliyepoteza watoto wake watano waliokuwa kwenye jengo lililo kule. Bado anasubiri kwa matumaini, ingawa matumaini hayo yanazidi kufifia, kwamba huenda watoto wake bado wakapatikana wakiwa hai. Kwa hiyo, tupo hapa katikati ya vifusi na harufu ya miili ya waliopoteza maisha, tukijitahidi kuwafikishia manusura chakula, maji na huduma za matibabu, huku tukiwasaidia kuanza kufikiria namna ya kujenga upya maisha yao. Lakini safari ya kurejea katika hali ya kawaida bado ni ndefu sana.”wakati huu ambapo ripoti za vyombo vya Habari zinaeleza kuwa jeshi la Marekani usiku wa kuamkia leo limekamilisha awamu mpya ya mashambulizi dhidi ya Iran, yakilenga zaidi ya maeneo 80 zikiwemo meli tatu za kibiashara zilizokuwa zinapita Mlango wa Bahari wa Hormuz huko Ghuba ya Uajemi, Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Bahari, IMO Arsenio Dominguez amelaani mashambulizi hayo mapya akionya kuwa kwa mara nyingine maisha ya mabaharia wasio na hatia yanawekwa hatarini.Na katika kujifunza lugha ya Kiswahili hii leo mtaalam wetu Onni Sigalla, Mhariri mwandamizi wa Baraza la Kiswahili la Taifa nchini Tanzania, BAKITA. Anafafanua maana za neno "KICHAKATA MATINI".Mwenyeji wako ni Anold Kayanda, karibu!