Jaridani leo tunakuletea mada kwa kina inayotupeleka nchini Kenya kumulika umuhimu wa wahisani. Pia tunaangazia siku ya Wahudumu wa Kibinadamu Duniani tukikuletea ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaomulika haki zao, na hali ya usalama nchini DRC.Leo ni Siku ya Wahudumu wa Kibinadamu Duniani na Umoja wa Mataifa unasema mwaka 2024 ulikuwa mbaya zaidi, baada ya wahudumu 383 kuuawa kote duniani, hasa Gaza na Sudan. Mratibu wa misaada ya dharura wa Umoja wa Mataifa, Tom Fletcher, amesema “Hata shambulio moja dhidi ya mhudumu wa misaada ni shambulio dhidi yeto sote.” Naye Katibu Mkuu António Guterres ameongeza kuwa “Shambulio dhidi ya wahudumu wa misaada ni shambulio dhidi ya ubinadamu hebu tuchukue hatua kwa ajili ya ubinadamu.Huko Geneva Katika hafla maalum ya kuadhimisha siku hii, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Volker Türk, amewakumbuka waliopoteza maisha, wakiwemo wahudumu 22 waliouawa Baghdad mwaka 2003, na kuongeza “Kamwe hatutaacha kusisitiza kwamba serikali au nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wafanye kazi pamoja kuhakikisha wanatoa fursa ya ufikiaji wa kibinadamu kwa watuwenye uhitaji na kunakuwepo na uwajibikaji wa ukiukwaji mkubwa wa sheria za kibinadamu zikijumuisha ulinzi kwa wahudumu wa kibinadamu na wa Umoja wa Mataifa”.Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, MONUSCO, leo umelaani vikali mashambulizi ya kundi la waasi wa Allied Democratic Forces, ADF kati ya tarehe 9 na 16 Agosti, katika maeneo ya Beni na Lubero, mkoa wa Kivu Kaskazini, yaliyoua raia 52, wakiwemo wanawake na watoto. Mashambulizi hayo yamehusisha utekaji nyara, uporaji, na uchomaji wa nyumba na magari, na kuwaacha wakazi ambao tayari wako katika hali ngumu ya kibinadamu katika mateso zaidi.Na katika mashinani na ikiwa leo ni siku ya wahudumu wa binadamu, huduma na kujitolea kwa wanachama 270 wa Kikozi cha Polisi cha walinda amani kutoka Ghana wanaohudumu katika Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS), wakiwemo maafisa wanawake 63, ilitambuliwa kwa kutunukiwa Nishani ya Umoja wa Mataifa ya Heshima kwa juhudi zao, zikiwa ni pamoja na kuwalinda raia, kuwezesha uwasilishaji salama wa misaada ya kibinadamu, kukuza haki za binadamu na kujenga amani. Bismark Achaab, Msimamizi Mkuu wa Kitengo hicho anatoa shukrani.Mwenyeji wako ni Anold Kayanda, karibu!